Wadudu-ute ni viumbehai vinavyofanana na nyungunyungu wafupi na wanene. Wana mnasaba na vidudu-dubu na arithropodi. Jina lao linarejea uwezo wao wa kurushia ute katika vitundu viwili vya matezi nyuma ya mdomo ili kujitetea au kukamata mawindo.
Mwili wa wadudu-ute umerefuka na una mapingili mengi. Kila pingili linabeba jozi la miguu isipokuwa mapingili matatu ya kichwa. Tofauti na arithropodi miguu hii haina viungo lakini ni kama vifuko vilivyojaa na hemolimfi (“damu”). Inaweza kusogea kwa msaada wa musuli chini ya ngozi. Kichwa kinabeba vipapasio viwili kwenye pingili la kwanza, lakini hivi havina homolojia na vile vya arithropodi. Pingili la pili lina kipenyo kinachofanya kazi ya mdomo lakini, tena, hiki hakina homolojia na mdomo wa arithropodi. Kuna mataya (mandibili) mawili yenye ncha kali katika mdomo. Vitundu vya matezi ya ute vipo kwenye pingili la tatu.
Ngozi ya wadudu-ute ina tabaka la nje la kitini na tabaka la ndani la seli. Chini ya ngozi kuna matabaka matatu ya musuli. Nje ya ngozi inabeba nywele fupi zinazokupa hisi ya mahameli (asili ya jina la kiingereza velvet worm).
Wasomaji wanaombwa kuchangia mawazo yao kwenye ukurasa wa majadiliano ya makala.
Kamusi za Kiswahili hazina jina kwa mnyama huyu au wanyama hawa.